Sunday, September 19, 2010

SASA UMEKUWA KIUMBE KIPYA

SASA UMEKUWA KIUMBE KIPYA
2WAKORINTHO 5:17
‘Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa Mapya.’
__________________________________
Salaam katika Jina la Yesu!
Ndugu msomaji.

Ni dhahiri wala sio siri ‘UKIOKOKA UNAFANYIKA KUWA KIUMBE KIPYA’. Mambo yote ya zamani (katika dhambi yaletayo uadui na Mungu) yamepita (yamefutwa/yameondolewa/yametupwa nje) na tazama YOTE yamekuwa MAPYA! Hilo ndilo Neno la Uzima Mpya: Kufanyika kuwa KIUMBE KIPYA!

Mara nyingi nimekuwa nikiwasikia baadhi ya watu (hata walio katika madhehebu ya Kikristo) wakisema ‘haiwezekani kuokoka ukiwa duniani’. Kwa jinsi ya kibinadamu ni kweli kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kujiokoa. Lakini kulingana na Biblia inavyoufunua ukweli wa kazi ya Yesu pale msalabani Wokovu ni SASA, LEO, WAKATI HUU! (2 Wakorintho 6:1-2).

Neno linasema ‘usipokee neema ya Mungu bure! Kwa lugha nyingine ‘neema’ ambayo Mungu ameileta kwa njia ya kifo cha Kristo na kufufuka kwake haikuletwa iliikae bure bila kutendewa kazi. Yakupasa kuichukua (appropriate the Grace of God Now!)
Yesu hakwenda msalabani pasipo sababu au pasipo matokeo ya kile alichokiendea! La hasha. Aliimaliza kazi na kulipa kila madai na hitaji la adhabu ambayo tuliistahili kwa sababu ya dhambi. Alipokuwa akifanya malipo hayo kwa njia ya mateso yake na alipokiendea kifo cha aibu msalabani, aweka tamko la hadharani akisema ‘IMEKWISHA’. Kwa lugha nyingine YOTE yaliyohitajiwa KULIPWA ili tupatanishwe na MUNGU na KUINGIA katika USHIRIKA MPYA na MUNGU YAMELIPWA KIKAMILIFU!

Ili mtu yeyote aweze kufaidi mbaraka wa Mungu unaoambatana na yale ambayo Kristo aliyaleta kwetu kwa njia ya kufa na kufufuka (Gal.3:13-14) (Isaya 44:3) kwake ni LAZIMA KWANZA UFANYIKE KIUMBE KIPYA!

Labda utauliza: Je inakuwaje kufanyika kiumbe kipya? Swali hilo ni zuri na wengi wamewahi kuliuliza. Ukisoma Yohana 3:4 utamwona mwalimu mmoja wa Torati akihoji inawezekana je? Ndiyo! Inawezekana: maana yote yanawezekana kwa yeye aaminiye! (Mk 9:23). (Taz. Pia Luka 1:37). Wokovu ni neema ya bure tuipokeayo toka kwa Mungu kwa njia ya IMANI katika Kristo. Kule tu kusikia Injili isemavyo na kumkubali Kristo kama mwokozi huleta mabadiliko ya PAPO KWA PAPO!

Ndiyo maana 2Wakorintho 5:17 inasema mambo muhimu yafuatayo:
1. Ikiwa.... (ikiwa nini?)...
2. Mtu (mtu gani? Yeyote? bila kijali alivyo?) Ndiyo! Yeyote..hata wewe!
3. Akiwa (wapi?)...
4. Ndani ya Kristo (sio ndani ya dini? La).
5. amekuwa (saa hiyohiyo? ).(Ndiyo).
6. kiumbe (maana yake kuna badiliko la ndani la kiuumbaji)..
7. kipya. (maana yake kuna kiumbe cha zamani kimetolewa/kuna kufanyika/ kuna kuzaliwa upya, mara ya pili (Yohana 3:3) (Yohana 1:12).

Kufanyika kiumbe kipya ni Muujiza wa kipekee sana ndani ya mtu! Ni jambo linalowezekana pale tu mtu anapoingia ndani ya Kristo. Unaweza ukawa na dini na ukasifika kama muumini mzuri. Lakini kuwa ndani ya dina hakukufanyi kuwa kiumbe kipya! Ndio maana hutaona badiliko lolote hadi utakapoingia kaburini! Wengi walioko magerezani kwa makosa mbalimbali kama vile uuaji, ubakaji, wizi, ujambazi, ulawiti, ulevi nk si kwamba hawana dini zao. Wote wako ndani ya dini moja au nyingine! Lakini kuwa ndani ya dini sio ndani ya Kristo.

Sasa utauliza: Je niweje ndani ya Kristo? Kitu gani kiniingize ndani ya Kristo? Wokovu (Kuokoka) ndiyo tiketi ya kukuingiza ndani ya ushirika na Kristo. Najua utauliza bado: sasa niokokeje? Swali lako si jipya. Liliulizwa kwanza kule Efeso na askari mmoja wa Kirumi aliyekuwa mlinzi wa gereza. Huyu alitaka kijiua! Lakini kwa vile neema ya Mungu ilikuwa imeingia ndani ya Gereza lake kuponya wala si kuamngamiza Ukisoma Matendo 16:28 Mtume Paulo alipaaza sauti yake akasema: USIJIDHURU!

Na kweli, wengi sana leo hii wamekata tama ya maisha na wana taka kujiua! Wengine wanataka kutoa mimba ambayo aliipata bila kutarajia na sasa anataka kuficha uhalisia wa maisha aliyokuwa akiishi (uzinzi/uasherati) kwa kuitoa mimba hiyo! Sikiza rafiki: USIJIDHURU! Iko nafasi ya kuyafanya mambo yako yote kuwa mapya! Unaweza kusamehewa na kuanza UPYA ndani ya YESU! Ukisoma Matendo 16:30, utaona swali lile muhimu ambalo umekuwa ukijiuliza: Nifanye nini basi nipate KUOKOKA? Paulo na Sila walilijibu swali hilo kwa ushauri huu ambao ni wa Mungu mwenyewe: ‘MWAMINI BWANA YESU, NAWE UTAOKOKA, PAMOJA NA NYUMBA YAKO!

Haya ni maneno muhimu sana kwako LEO! Huna haja ya kukata tamaa juu ya maisha yako ya nyuma. Huna haja ya kujiangamiza au hata kumwangamiza mtoto huyo aliyeko tumboni mwako! Iko njia sahihi ya kukuponya wewe na nyumba (mtoto) wako! Ni njia rahisi kabisa: AMINI LEO! MPOKEE YESU LEO! Atayafanya upya maisha yako! Atakufanya KIUMBE KIPYA! Inawezekana.

Tena, Biblia yasema hivi: TAZAMA!
1. Mambo yote ya kale yanaondolewa
2. Tazama YOTE yamekuwa Mapya!
Mpendwa wangu, Kuwa ndani ya dini (hata kama ni ya Ki-Kristo) sio kuwa ndani ya Kristo. Ukristo (Wokovu) na Dini ni vitu viwili tofauti. U-Kristo ni ushirika na Mungu NDANI ya Kristo Yesu. Dini ni utaratibu wa watu kumtafuta na kutumikia kile wanachoamini ni ‘mungu’. Ndani ya dini kuna ‘taratibu’ au sheria na kanani za kufuata katika kumtafuta huyo ‘mungu’ na ‘msaada wake’ kama anaweza kuutoa! Hakuna ushirika. Lakini ndani ya Kristo kuna ushiriki. Mara tu unapokuwa ndani ya Kristo unaingizwa katika ushirika na Mungu. Mungu anahamia ndani yako! (2Wakorintho 6:16 inasema hivyo!)

Kama hujampokea Yesu Kristo na KUOKOLEWA Unangoja nini? Waweza kuokoka sasa, mara hii unaposoma makala hii! Kama wajua hakika ya kwamba huja okoka na hauko ndani ya Kristo bali una dini tu waweza kufanya uamuzi na kufanya toba nomba toka moyoni mwako rehema za Mungu na neema ya WOKOVU nawe UTAKOKA! Ukiamini:
Sala hii yaweza kukusaidia:

‘Bwana Yesu, ninakuja mbele zako. Ninatubia uovu na dhambi zangu na kutokukuamini kwangu. Naomba unisamehe leo. Nakupokea Moyoni mwangu. Takasa Maisha yangu kwa Damu yako. Asante kwa kunisamehe na kunifanya mwanao Leo. Sasa mimi nimeokoka! Asante Yesu kwa kuniokoa! AMINA!
(Na kweli: SASA UMEKUWA KIUMBE KIPYA
Wasiliana name: nangela04@yahoo.co.uk
Mobile: +255-755-654 129.

No comments:

Post a Comment