‘KULIIMARISHA AGANO’
Kumb: 8:11-19
‘BALI utamkumbuka BWANA Mungu wako , MAANA NDIYE AKUPAYE NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI; ILI alifanye IMARA Agano lake ....’
Mpendwa Msomaji wangu!
Salamu nyingi tena katika Jina lile zuri tulilopewa; Jina la Yesu!
Karibu katika wakati mwingine wa ‘Makala ya Baraka’.
1. UTANGULIZI
Leo tunajifunza juu ya ‘Kuliimarisha Agano’. Agano ni makubaliano baina ya pande mbili upande mmoja ukiwa na mamlaka zaidi lakini ukujishusha na kufikia makubaliano ambayo yana kanuni zinazowafunga watu wote wiwili. Pamoja na kuwa ni ‘mkataba’ agano lina nguvu zaidi kuliko mkataba wa kawaida. Ndani ya agano kuna viapo. Katika utaratibu wa jamii nyingi agano lilifungwa kwa damu! Hata katika Israeli watu waliingia katika agano la damu kwa kumchinja mnyama na kumpasua vipande viwili kisha kila upande kupita katikati yake kama ishara ya kuingia makubaliano na kuapiana kutoyakiuka.( Bwana alifanya hilo na Ibrahim (Mwa.15:8-18). Katika agano mafanikio yako ni mafanikio yangu. Na Mafanikio yangu ni mafanikio yako. Taabu yangu ni taabu yako na taabu yangu ni taabu yako. Vita vyako ni vyangu na vita vyangu ni vyako. Adui zangu ni adaui zako nk. Kulikuwako na namna mbalimbali za kuthibitisha maagano. Mfano mwingine mzuri ni agano la Daudi na Mwana wa Sauli Yonathani. (1Sam.18:1-4). Yonathan alimpenda Daudi kama nafsi yake mwenyewe. Naye Daudi aliliheshimu hata baada ya kifo cha Yonathan bado Daudi alimtendea mema mwanaye –yule mlemavu Mefiboshethi. (2Sam. 9:1, 7)
Katika kipindi chetu cha Agano Jipya Mungu pia ametupenda kuliko upeo na kuingia katika Agano na sisi yeye mwenewe alilithibitia na kulitia muhuri kwa njia ya Kifo cha Kristo Yesu Mwanawe wa pekee.(Yoha.3:16 inasema ‘kwa maana jinsi hii (yaani mateso na kufa kwa Yesu msalabani) Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe pekee ...” Sharti moja katika agano hili ni ‘Imani’ kwa huyo aliyemtoa kwa ajili yetu ‘yaani’ YESU. Ndani ya Agano hili kuu zipo ahadi na Baraka tele. Hata hivyo Baraka na mafanikio yaliyopo yana malengo na makusudi maalumu. Hapa ndipo tunapo anzia katika somo letu la leo.
2. LIPOKUSUDI LA MUNGU KUKUFANIKISHA
Mungu hutufanikisha kwa kusudi maalum. Yanipasa/yakupasa kujua hilo. Mafanikio yako ya kifedha, kielimu, kiuchumi, kibiashara, kiafya, kifamilia, kihuduma nk si kwa ajili yako binafsi wala usijitwalie utukufu kwa hilo! La hasha! Ni kwa ajili ya kusudi maalumu ambalo ni hili: ‘Kuliimarisha' Agano la Mungu na Wewe. ‘Hukuokolewa bure (yaani bila sababu) na pia hufanikishwi bila lengo!
Katika fungu la maandiko yaliyopo kwenye mistari tajwa hapo juu (Kumb.8:11-19) Bwana anaanza na TAHADHARI.
Anasema: (Mstari wa 11-19:
‘‘JIHADHARI’, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, na kutozishika amri zake, na hukumu zake ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulichonacho kitakapo ongezeka; basi hapo MOYO wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako, apate kukutweza, apate kukujaribu, iliakukutendea mema mwisho wako.
Hapo usiseme MOYONI mwako , Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. BALI utamkumbuka BWANA Mungu wako , MAANA NDIYE AKUPAYE NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI; ILI alifanye IMARA Agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. Lakini itakuwa, kama ukimsahau BWANA, na kuiandama miungu mingine na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia LEO ya kuwa mtaangamia bila shaka (hakika).’
Tuanzie hapo na tujiulize maswali kadhaa:
• Je ni kwa nini Bwana anasema tujihadhari?
• Je mtu aweza kumsahauje Bwana (au) ni mambo gani yanayoweza kumfanya mtu akamsahau Mungu na Neno lake (amri zake) ?• Ni mazingira gani ambayo kwayo Bwana alitoa maonyo haya?
Labda tuanze na swali la mwisho la mazingira au muktadha (context) yaliyopelekea Bwana atoe angalizo hili! Kwangu mimi naliona hili ni angalizo linalobeba ‘Siri’ ya kuendelea vizuri na kuendelea kufanikiwa ukiwa ndani ya Kristo au ndani ya Wokovu.
Lengo kubwa la kitabu cha Kumbukumbu la Torati lilikuwa ni kuwakumbusha wana wa Israeli yale yote ambayo Bwana aliwafanyia na kuwatia moyo (ikiwa ni pamoja na kuwatahadharisha) kuhusu ‘umuhimu wa kujiweka wakfu upya kimaisha kwa Bwana’. Mambo haya wana wa Israeli wanaambiwa wakiwa ngambo yam to Yordani (kabla hawajavuka kuingia kwenye mbaraka wa Bwana aliowaahidia! Wamekwisha sota Jangwani kwa miaka kadhaa na sasa wapo ukingoni mwa ‘kutoboa maji’. Kwa lugha nyingine ni kama vile mchimba madini aliye karibia kutoboa mwamba wenyewe wa dhahabu tupu!Karibu shimo lianze kutema baada ya muda mrefu wa kusota na jasho jingi kumwagika! Kwa wale waliooa/olewa ni kama usiku mmja tu kabla ya kuingia kwenye ‘siku yenu’ mliyo ingojea sana kwa shauku na matarajio. Hebu piga picha! Kunakuwepo na tashwishi Fulani na matazamia makubwa yanayofunika hata ule muda mreeefu wa kusubiri! Katika hali hiyo ndipo Bwana analeta ‘ANGALIZO!’ Ana waambia ‘Jihadharini msije mkanisahau au mkasahau sheria yangu!’ Kwa ufupi hiyo ndio muktadha ya kitabu hiki cha Kumbukumbu la Torati na msingi wa sura hii ya Nane.
Sasa turejee katika maswali mawili yaliyobakia: Je mtu awezaje kumsahau Bwana?
Yapo mambo kadhaa ambayo nimeyatilia mkazo katika maadiko tuliyosoma hapo juu. Mpendwa mafanikio ni kitu kizuri sana na Mungu anapenda kila mtu afanikiwe.Katika (3Yoh 1:2) tunaona hilo: Ansema “ Mpenzi (yaani ewe liye pendawa!) naomba ufanikiwe katika mambo YOTE na kuwa na AFYA yako!” Ni makusudi ya Mungu tufanikiwe tena tuwe na afya zetu kikamilifu. Tena kama tulivyoona yeye Bwana ndiye anayehusika na kutufanikisha kwa kutupa ‘nguvu’ (anointing) (upako) wa kufanikiwa! (Lakini kumbuka upako hauji bila kusudi! Mdo: 1:8’.... mtapokea ‘nguvu’....nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika....’)Hayo ndiyo masharti ya upako! Na ndivyo yalivyo ya upako wa mafaniko!
Katika mambo niliyotilia mkazo hapo juu kwenye andiko letu la somo utaona kitu cha kipekee! Bwana anatoa tahadhari. Anasema kuwa MAFANIKIO ni kitu cha kuchukulia kwa TAHADHARI. Kwa nini? Kwa vile yana uwezo mkubwa sana wa kukutoa kwa Mungu! Baraka zinaweza kukufanya ukamsahau Mungu kuliko shida! Mara nyingi shida hukuleta kwenye magoti! Lakini si rahisi kwa mafanikio kukuleta kwenye magoti, japo ndivyo inavyotakiwa iwe! Kama hujajifunza somo kama hili hutaelewa. Lakini nataka leo tujifunze pamoja na tuelimike kwa kuupata ujuzi huu wa kweli ya Mungu kwamba: MAFANIKIO YANATAKIWA YAKULETE KWENYE MAGOTI ZAIDI KULIKO HATA SHIDA! Kwa lugha nyingine wakati ufanikiwapo ‘mtafute Mungu’ zaidi kuliko kabla ya kuyapata! Tafuta kuujenga ushirika na Mungu zaidi kuliko awali! Hii ndiyo siri ambayo wengine walipoikataa walijikuta wamefunikwa na mafanikio yao wakamsahau aliyewapa yaani Mungu!
Bwana anasema: Chukua tahadhari :
(a) Wakati umekula ukashiba (yaani unachakula chakukutosha)
(b) Umejenga nyumba (wewe si ‘homeless’).
(c) Makundi yako yameongezeka (biashara, una assets mbalimbali, elimu ya kiwango kizuri nk)...
(d) Fedha yako na dhahabu imeongezeka...(una uhakika wa mshahara mzuri au akiba unayo benki..nk)
Basi chunga sana ‘ Moyo wako’! Oh! Moyo, moyo wa mwanadamu mpendwa ni kitu cha ajabu sana! Wakati fulani tajiri mmoja alikuwa na magari mawili mapya, mazuri. Yalikuwa magari yake ya kwanza katika maisha yake kuwahi kuyanunua. Siku moja akawa anayasafisha na anayaangalia. Ghafla moyoni akajiambia ‘du! Yaani na mimi nina magari mawili! Ama kweli...” Wazo hilo la kujisifia lilimpa fundisho maana siku si nyingi gari moja na upya wake likapata ajali mbaya na kuharibiwa vibaya! Ndipo alipozinduka na kugundua kuwa ‘moyo’ wake ulikuwa unatukuka na kupoteza mwelekea sahihi ikambidi atubu mbele za Mungu wake! Je wamkumbuka Nebukadreza? Jinsi alivyojitukuza? Soma mwenyewe (Dan 4:28-33).
Biblia inasema katika Yeremia 17:9-10 “ Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nnani awezaye kuujua? Mimi ,Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.’
Mafanikio ni kitu kimoja ambacho kinaweza kuugeuza moyo wa mtu ukadanganyika na kujitukuza juu ya kazi ambayo aliyeifanya ni Mungu wala si wewe. Tuangalie tena habari ya mfano wa mtu mmoja.
‘Mwana kijiji mmoja alikuwa ameokoka. Hakuwa na mali yoyote, tena kwa kweli, alikuwa maskini tu na mhitaji. Lakini alikuwa mwombaji na hakukosa ibada hata moja Jumapili na katikati ya wiki. Alikuja na Biblia yake kwenye kamfuko alikokaning’iniza begani kila siku! Hakutembea barabarani bila kamfuko kake na Biblia yake ndani yake ili apatapo hata fursa kidogo asome Neno au ashuhudie habari za Yesu. Alikuwa na bidii na mambo ya Mungu. Katika familia yake alikuwa hana kitu ila yeye, mkewe na binti zake wawili. Ilikuwa familia ya watu wa Mungu wanaoishi kwa kumtegemea Bwana. Siku zikapita na miaka ikaenda. Kwa neema binti zake wakakua na wakapata wachumba na kuolewa. Mahari zikaletwa, na moja ya sehemu ya mahari ile ilikuwa ng’ombe wanne. Tayari Mzee yule akabadili maisha yake maana sasa pale kijijini akawa mmoja wa watu wenye mali na ng’ombe wake wakaanza kuzaa na kuongezeka. Lakini jambo moja baya kwa upande wake ni kuwa mara baada ya kupata utajiri wa ng’ombe Mzee yule akaanza taratibu kutoonekana kanisani na ibadani. Yuko wapi? Yuko ‘bize’ na fimbo begani (sio tena mfuko wa Biblia) akichunga ng’ombe wake. Mwishowe akaacha wokovu kabisa! Moyoni aliweka ng’ombe akamsahau aliye mpa hao ng’ombe!
Mpendwa wangu,
Jambo hili ni rahisi kutokea hata katika mazingira mengineyo yasiyofanana nay a kupata ng’ombe!
Kama hukuchukua tahadhari ni rahisi mno kumwacha Bwana kuliko unavyofikiri . Ni rahisi mno kujivuna na kujiambia ‘la lakini nilikuwa nafanya bidii wewe! Ndio maana nikafanikiwa namna hii!’ SAWA! Ulikuwa na bidii, na Bwana anatakila kila mtu awe na ‘bidii ilele’ wala usiwe mvivu (Waebrania 6:11-12); lakini kumbuka kuwa ni Bwana ndiye akupaye nguvu, afya, mawazo mapya nk ili kupata hicho ulichopata. Kwa hiyo MTANGULIZE YEYE, MJULISHE KWA WENGINE KUWA YEYE NDIYE ALIYEKUFANYIA!
Je umegundua kitu mpaka hapo? Ni kitu gani kinachoweza kukufanya ukamsahau Bwana? Jibu ni rahisi: MAFANIKIO.
3. SASA TUFANYEJE ILI MAFANIKIO YASITUTOE KWENYE UWEPO?
Kumb.8: 17 inasema: ‘Utamkumbuka Bwana, Mungu wako MAANA NDIYE AKUPAYE NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI.
Nilipokuwa nasoma habari za Yakobo alipotoka kwa Labani na Mali, ng’ombe, kondoo, punda, ngamia, wafanyakazi kemkem na watoto na wake zake, niligumdua kuwa mara alipokutana na ESAU kaka yake, Esau alipomuuliza ‘nini hii yote na hawa ni akina nani’ YAKOBO alijibu jibu la mtu aliyekutana na MUNGU na kujua kuwa kwa kweli katika hili si mimi wala sina mkono ndani yake hata nijivune! Ukisoma Mwanzo 32: 9-10 utaona maombi na ukiri wake mbele za Mungu na jinsi alivyosema baadae na Esau. Anasemaje YAKOBO mbele za BWANA:
‘Yakobo akasema,Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, “Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, name nitakutendea mema”; mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili!...’
Ukisoma alipokutana na Esau katiika Mwanzo 33:5 Esau alimuuliza : ‘...Ni nani hawa pamoja nawe?’ Tazama majibu ya Yakobo: (mstari wa 5b) ‘Akasema: ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake.’ Mtu huyu alimjua BWANA na kutambua kuwa kama si Mungu na Neema yake, hangalikuwa na kitu! Hivyo aliimtambulisha Mungu na Neema yake kwa watu kuhusu mafanikio yake. Tazama tena majibu yake kwa Esau kuhusu zawadi alizotuma kwake (Mwanzo 33:8 Esau anauliza : ‘Kundi hili lote nilililikuta maana yake ni nini?’ (alishikwa na butwaa). Naye Yakobo ana mtambulisha Mungu kwa habari ya mbaraka alioupta anasema (Mwa: 33:11 ‘ Pokea tafadhali mbaraka wangu, ulioletewa kwa sababu MUNGU amenineemesha...’ (Nani aliyemneemesha: Mungu!).
Mithali 8:17-21 inaweka bayana kuwa Mungu ndiye mwenye utajiri wote na kuwa ndiye awarithishaye mali wale wampendao. Tunarithishwa maana sis ni watoto wake na warithi turithio pamoja na Kristo. (Gal.4:6-7).
Hivyo basi: Ilikuepuka kumsahau BWANA au kuepuka uwezekano wa kufunikwa na Baraka hata ukamsahau Mungu: CHUKUA TAHADHARI KILA SIKU! Jiambie mwenewe na yeyote akuulizaye kuwa ‘Ni BWANA aliyenineemesha’. Kumbuka hilo na kamwe usikubali shetani akusahaulishe! Wala Moyo wako usikudanganye! Mkabidhi Bwana Moyo wako 100% maana anasema ‘Mwanangu nipe moyo wako!(Mithali 23:26)’ Timiza wajibu wako kwa Bwana. Kwa mfano wengine wanapofanikiwa sana wanaacha kutoa mafungu ya kumi. Na ni rahisi mno kuacha maana kama biashara imekubali ukafikia kupata , kwa mfano faida ya million 100, je ni rahisi kuto milioni 10 kama zaka? Moyo huwa mdanganyifu sana katika hili. LAKINI nakuambia toa hata kama ni bilioni! Usitekwe na adui kusema ‘lakini zote hizi mh?’ Bali utamkumbuka Bwana...’ itakusaidia. Kumtanguliza Mungu na kushika sheria (Neno) lake ni dawa ya kushinda kishawishi cha kufunikwa na mbaraka hata ukamsahau aliye kubariki. Lakini yakupasa kujifunza haya na kuyatendea kazi.
4. UTAJIRI (MAFANIKIO) YAKO NI KWA AJILI YA AGANO!
Kusudi la Mungu kukufanikisha ni ili wewe uliimarishe AGANO lake. Kuimarisha maana yake ni kufanya kitu kiwe imara zaidi au kisitikisike kinapopitishwa au kukumbana na mikikimikiki. Urafiki uliimarika ni ule wa kushibana sawasawa. Pete na kidole waswahili wanasema. Ukiondoa kimoja na chapili nacho kitaondoka! Kadiri tunavyo uonesha upendo wetu kwa Yule tuliye naye katika agano ndivyo linavyozidi kuimarika! Hata katika agano la ndoa, kwa mfano, kadiri mnavyoendelea kupendana ndivyo mnavyozidi kufanana hadi mnafikia mahali pa kuwaza kitu kilekile kimoja! Kila agano halina budi liimarishwe.
Tunaweza kuliimarisha agano letu na Mungu kwa kutimiza yale mashari tuliyokubaliana na Mungu alipotuokoa. Wote tulimwahidi Mungu kumtimikia kwa Mioyo yetu YOTE, Nguvu zetu ZOTE na Akili yetu (nafsi yetu) YOTE. Hii ni pamoja na mali, fedha,elimu , biashara nk. Vyote hivi ni lazima vilenge kutimiza mkusudi ya Mungu. Kama ni elimu umepata basi angalia itumie kuujenga Ufalme. Kama ni fedha au nafasi yoyote uliyo nayo kumbuka Mungu amekuweka mahali ulipo, nafasi uliyo nayo na kila kitu ili UMKUMBUKE BWANA MUNGU WAKO kwa kutenda sawasawa na sheria yake! Toa ulivyo navyo kwake, mafungu ya kumi, sadaka na matolea, misaada kwa wenye uhitaji, fadhili kazi ya Injili kwa bidii, fanya kitu katika ufalme maana wewe ni wakili tu wa mali ambazo Mungu ameziweka mikononi mwako.
5. MWISHO:
Kumbuka siku zote ya kwamba ukijisahau na kuzitumikia mali badala ya Mungu. Ukijisahau elimu yako ikachukua nafasi ya Mungu, fedha na biashara yako ikachukua muda wako na Mungu kama Yule mzee na ng’ombe wake wanne, BWANA anashuhudia akisema : ‘UTAANGAMIA BILA SHAKA’ maana hiyo mali itakuwa na mafanikio yatakuwa ‘TANZI’ badala ya ‘BARAKA’ kwako nawe ‘UTAANGAMIA bila shaka! Mali yaweza kugeuka ikawa ibada ya sanamu! Elimu yaweza kuwa ibada ya sanamu! Cheo nk vyote vyaweza kugeuka kuwa ibada ya sanamu kama havitakabidhiwa katika mikono ya BWANA aliyekupa. Hivyo mpendwa wangu:
JIHADHARI...na MKUMBUKE BWANA MUNGU WAKO (Ufanikiwapo) Maana ndiye akupaye NGUVU za kupata UTAJIRI ili kusudi ALIIMARISHE AGANO LAKE (na wewe) ndani ya Kristo!
Hadi majira mengine tukijaaliwa na Bwana,
Kaa na Amani ya Kristo,
Ni mimi mjoli wako,
Mwinjilisti Deo John Nangela,
No comments:
Post a Comment