Tuesday, June 6, 2017


"MAISHA NI NYUMBA NA NYUMBA NI MSINGI"

Luka 6:46-49

Sehemu ya I
Bwana Yesu asifiwe!

Ndungu msomaji wangu nakusalimu katika Jina la Yesu. Ni muda mrefu lidogo tangu niandike ujumbe wa kukutia moyo katika blogu hii ya ONLY BELIEVE! (AMINI TU!). Hata hivyo namshukuru Mungu kuwa nimerejea tena.

Upo msemo mmoja ambao umekuwa ukitumiwa sana na shirika moja la umma nchini Tanzania katika kunadi bidhaa zake. Msemo huo husemwa hivi: "Maisha ni Nyumba"- wakimaanisha kuwa kama hujajenga nyumba basi maisha yako yako katika hati-hati ya mahangaiko ili-hali wao wanaweza kukupatia nyumba ya bei nafuu kabisa, ukaishi maisha yenye utulivu, ukapanga mipngo yako na kuendelea mbele kimaisha. Kwa hali hiyo wao hujinadi kwa kusema : Maisha ni nyumba!

Katika hali ya kuutafakari msemo huo ndipo nilipopata nafasi ya kulitafakari Neno la Mungu lisemavyo na kuona kuwa maisha ya mtu wa Mungu, mtu wa roohoni yaani Mkristo ni Nyumba inayojengwa kila siku na Numba inakuwa Nyumba kutokana na Msingi wake. Hivyo Nyumba ni Msingi. Kulianagali jambo hilo kimaandiko na kuona ni jinsi gani tunapaswa kuyajenga maisha yetu ya Ki-kristo, tuangalie Maandiko Matakatifu katika Injili ya Luka 6:46-49.

Yesu alifundisha akisema maneno haya:
"Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo? Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa."

Kwa kuchukulia ule msemo wa 'maisha ni nyumba'  na kwa kuyaangalia maandiko hayo yaliyonukuliwa hapo juu, utaona kwamba nyuma ni MSINGI. Bila kuwepo kwa msingi imara nyumba yoyote ile inayojengwa itaanguka tu- kama si leo basi baada ya muda si mrefu! Hili latufundisha nini basi?

Maisha yetu ya Ki-kristo yanafananishwa na nyumba inayojengwa. Mjenzi ni wewe au mim mwenyewe. Kila siku tunaijenga nyumba hii lakini ujenzi huu uko wa aina mbili , yaani ipo tofauti katika kujenga kwetu.

Kwa upande mmoja wapo wale ambao wanajenga maisha yao ya kila siku juu ya msingi ulio imara, usioweza kutikiswa na kitu chochote- yaani wanajenga juu ya NENO LA MUNGU. Neno la Mungu yaani "Biblia" ni mwamba ulio imara sana ambao hauwezi kutikisika au kutikiswa na jambo lalote au halitabia yoyote. Hii ni kutokana na tabia ya Neno lenyewe.

Kataka Zaburi ya 12:6 Biblia inasema hivi kwa habari ya uthabiti wa Neno la Mungu. Inasema, nami nanukuu:
"Maneno ya BWANA ni maneno safi. Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; iliyosafishwa mara saba."
               Mithali 30:5 inasema

               "Kila Neno la Mungu limehakikishwa.       
                Zabiri 18:30  yasema:

               "Ahadi ya BWANA imehakikishwa".
Katika kujenga maisha thabiti juu ya NENO la Mungu, Yesu alifundisha pia juu ya mambo kadhaa muhimu kuyazingatia na kujipima kwayo kadri tunavyoenenda siku kwa siku. Moja ya mambo haya ni 'Kusikia Neno' na 'Kulitenda Neno'.

Kusikia Neno : hii ni hatua ya awali sana katika kujemga maisha ya Kikristo yenye matunda, kwa mtu anayemjia Kristo, yaani  mtu aliyeokoka. Ni vizuri, tena ni muhimu kulisikia Neno linavyosema na maisha yako au yangu , tena tulisikie kwa 'sikio la ndani' sana, yaani sikio la rohoni. Biblia inasema tulisikiapo Neno huleta kuliamini au Imani.

Warumi 10:17 inasema:
           "Basi imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa Neno la Kristo".

Hivyo,  kulisikia Neno la Kristo huleta kujengewa imani ndani yetu. Lakini kusikia tu haitoshi maana imani yapaswa kuwa na mizizi ndani ya mtu kwani tunakua na kuongezeka toka imani hata imani! Katika hili la kusikia kuna hatua ya ziada ambayo inaambatana na sio tu kusikia bali pia kulielewa Neno. Mtu aliyelisikia tu Neno la Mungu lakini asichukue hatua zaidi ya kutaka kulielewa Neno alilolisikia na kulipokea hatafaidika au halitamfaida kitu.

Yesu aliliweka bayana jambo hili katika Injili ya Luka 8:4-15 aliopoutoa mfano wa Mpanzi aliyekwenda kupanda mbegu. Mistari ile ya 11 hadi 15 Yesu anatoa ufafanuzi wa mfano alioutoa kwa wanafunzi wake. Katika tafsiri ile Yesu anaonesha waziwazi kuwa mtu anaweza kulisikia Neno la Mungu nalo likamfaidia au lisimfaidie kabisa.

Luka 8:11-12  Yesu anasema hivi:
"Mbegu ni Neno la Mungu. Wale waliopandwa karibu na njia ndio wasikiao kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo Neno mioyoni mwao wasije wakaamini na kuokoka."

Kama utakavyoona hapo juu, lengo la Neno la Mungu ni kumwokoa yule anayelisikia. Humpa mtu msaada wa kuvuka toka ng'ambo moja hadi ng'ambo ya pili. Yaani kutoka mautini kuingia uzimani (Yohana 5:24). Lakini ili hilo litimie kuna kuliamini Neno, jamba ambalo hija kwa kulisikia lakini si tu kulisikia bali na kutafuta kulielewa ili kuendelea kukaa katika hilo lililosikiwa bila kulionea mashaka. Kama mtuakisikia tu halafu asiendelee nalo, Yesu alitahadharisha kuwa "huja yule mwovu akaliiba, akaliondoa moyoni mwa mtu huyo" ili asije akaliamini na kuokolewa.
 
Kwa hiyo basi:  'Kusikia tu neno hakutoshi, tafuta kulielewa Neno la Mungu!'

 Tutaendelea tena tukijaaliwa neema!

Barikiwa sana na Bwana.

Ni mimi nduguyo katika Kristo, Mchungaji Dkt.Deo John Nangela

 

No comments:

Post a Comment