Wednesday, October 23, 2013


SIFA ZA UFALME WA MILENIA

Sehemu ya II.

Karibu tena ndugu msomaji wa blogu hii ya AMINI TU! (Only believe!) Katika somo lililopita tulijifunza juu ya Ufalme wa milenia na sifa zake. Habari za ‘Ufalme wa milenia’ zipo katika kitabu kile cha Ufunuo wa Yohana ukianzia Sura ya 19 hadi ya 20. (Tazama pia Waefeso 1:10)


Kwa leo tunaendelea na sehemu ya pili baada ya kuona kuwa sisi kama Kanisa la Kristo, tu mawakala wa ufalme wa Mungu.  Tuliona kuwa moja ya sifa za Ufalme wa Millenia ni Yesu mwenyewe kuwa mtawala kwa kipindi cha miaka 1000! (Ufunuo 20:4). Katika kipindi hiki sifa kubwa sana ni kwamba kutakuwa na amani kuu!
·         Amani Kuu- ni sifa ya ufalme wa MILENIA.

Katika Mika 4:1-2 na Isaya 2:4; na 51:11 Biblia inaweka wazi kuwa kipindi cha milenia kitakuwa kipindi cha amani tele tele! Tena inabaibisha wazi kwamba huzuni zote “zitakimbia”.

 ·         Ufahamu wa Ki-mungu- ni sifa nyingine ya kipindi hiki.

Kutakuwa na kunjua Mungu kwa namna ambayo kutaijaza dunia yote kipindi chote ambacho Mfalme Mkuu Yesu Kristo atakapo tawala pale Yerusalem –Israel. ( Isaya 11:1-9) (Dunia itajawa na kumjua Bwana kama maji yanavyoifunika bahari!)

·         Watu wote watayafanya mapenzi ya Mungu maana watamjua.

Hii nayo ni sifa ya kipindi hiki. Bwana atatawala kutokea Yerusalem na atatawala “kwa fimbo ya chuma” ikimaanisha atatawala kwa haki na hukumu. (Isaya9: 6-7; Mika 4:3).

Mwisho wa Ufalme wa Milenia ni baada ya miaka 1000 ya utawala wa Kristo hapa duniani. Baada ya miaka hiyo ufalme wa milemnia utachukua sura mpya ya “Ufalme wa Mungu”. Huu utadhihirika kwa matukio makuu matatu:

a)    Shetani atafunguliwa baada ya ile miaka 1000 ya kifungo chake (maana kipindi cha Millenia hatafurukuta) (Ufunio 20:1-3). Wakati huo atajipanga kufanya vita (a final show down) dhidi ya Bwana Yesu Kristo na watakatifu (wateule) lakini atashindwa kabisa katika vita hiyo kuu sana. Yapo mataifa ambayo yatashikamana na Ibilisi kupigana na Kristokatika kipindi hichi cha mwisho baada ya milenia lakini watashindwa – Ufunuo 20:7-10 inabainisha haya.


b)   Shetani (Ibilisi) atakomeshwa kabisa na ufalme wake utaondolewa na kukoma kabisa!

 
c)    Waovu wote watahukumiwa na kutiwa hatiani kwa yale yote yaliyotendwa katika mwili. Hii ni hukumu ya mwisho (tz.Ufunuo 20:11-15). Haya yote yatatokea wakati wa mwisho baada ya kipindi cha milenia kumalizika. Watu wote ambao hawataonekana katika “Kitabu Cha Uzima Cha Mwana-kondoo” watatupwa katika ziwa la moto, nah ii inaitwa “mauti ya Pili” maana watatengwa na Mungu aliye hai milele na milele!

Ni muhumu basi, ndugu msomaji wangu mpendwa, kuzingatia sana habari za wokovu huu tuliopewa. Maandika yanasema  sis je tutapata je kupona tusiojali wokovu huu? Kumbuka kuwa pazia la wokovu lilianza pale Eden na kudhihirika pale Golgotha! Baadae litakunjwa au  kufungwa baadaye – yaani Mungu ataufunga ukurasi wa maisha ya dunia hii. Je umesha fanya maauzi ya wapi utakuwa umeangukia? Je ni katika ziwa la moto au ni katika Paradiso ya Kristo? Katika hayo mawili unapaswa kuyafanyia maamuzi. Uamuzi wa kumchagua Yesu na kuingizwa katika kitabu cha Uzima cha Mwanakondoo ni wa maana zaidi kuliko kuishi bila uhakika wa maisha ya sasa na yale ya baadae.

Mungu akubarikie kwa kusoma na kuchukua hatua. Kwa maswali zaidi, niandikie: nangela04@yahoo.co.uk au fuatilia katika blogu hii.

Tuesday, April 2, 2013


UFALME WA MUNGU: SIFA ZA UFALME WA MILENIA

Utangulizi

 Karibu tena ndugu msomaji wa Blogu hii ya “Amini tu!” (Only believe!) . Salamu nyingi za Mwaka 2013! Ni mapenzi ya Mungu nikuandikie tena na samahani sana kwa kutokukuandikia katika kipindi cha takribani mwaka mzima wa 2012. Hata hivyo, namshukuru Bwana wa uzima wetu kwa neema yake nimerejea tena. Kipindi hiki naomba tishirikishane kweli za Biblia kuhusu –“UFALME WA MUNGU –KIPINDI CHA UTAWALA WA MILENIA- yaani miaka 1000”. (Ufunuo 20:3) Katika kipindi hiki shetani atakuwa amefungwa.
Ni nini maana ya Ufalme wa Mungu?

Moja ya mambo ambayo Biblia imeyasisitiza sana ni juu ya ujio wa Ufalme wa Mungu. Ufalme wa Mungu ni utawala wa Mungu kati ya/juu ya Wanadamu na uumbaji wa Mungu.  Katika dhana ya Ufalme wa Mungu ipo dhana ndogo ya Utawala wa Kristo wa Milenia. Huu ni ule utawala wa Bwana Yesu katika dunia hii kwa kipindi cha miaka elfu moja (1000) yaani milenia moja. Katika kipindi hiki:

                                i.            Kristo Yesu atatawala ulimwengu wote.

                              ii.            Israel wote watarejeshwa pale mashariki ya kati kikamilifu- yaani katika nchi yao ya ahadi (Palestine).  Twajua ya kini kwamba Mungu alishaanza haya tangu mwaka 1948 mara tu baada ya Israel kupata uhuru wake. Hata sasa Mungu yu kazini kuhusu kutimiza haya ambayo Neno lake lilisha yaweka wazi.

Maandiko

Tuanze na Nabii  Isaya 11:10-12. Hapa Bwana nasema atawatwekea mataifa bendera na wana wa –Israeli waliotawanyika watakusanywa toka pande zote nne za ncha za dunia. Kama tulivyobainisha hapo juu, Bwana alishaanza.

Yeremia naye hakuacha kusema juu ya jambo hili. (Yer.16:14-15). Mara ya kwanza Bwana aliwatoa Misri. Mara hii anawatoa katika utawanyiko pande zote za dunia.

Yer. 30:10 anasema Yakobo atarudi na kutulia.Maana Bwana ndiye aliyewapanda, nani atawang’oa?

Nabii Ezekieli naye analo la kusema. Ezek.36:24, na Ezekie 37 inasema wazi kuwa pamoja na kuwa Israel ilionekana kama bonde la mifupa, bado Bwana alitangaza maona haya kwa Ezekiel kwamba atawafanya kuwa Taifa kubwa na lenye nguvu.
Kipindi tuishicho

 Kipindi tuishicho sisi ni kipindi cha kipekee sana maana twayaona kwa macho ya nyama na damu (wazi-wazi) mambo mengi ambayo Mungu aliyasema kwa unabii siku za nyuma. Kuzaliwa kwa taifa la Israeli, kwa mfano, ni jambo ambalo Mungu alilitabiri miaka mingi hata kabla Yesu hajaja. (taz. Isaya 66:7-8). Tayari tunamwona Bwana aliwarejesha Israel toka nchi nyingine, mfano toka  Ulaya ya Mashariki, Urusi ya zamani , Africa (Ethiopia) n.k. Hata hivyo, Waisraeli walio wengi bado wanangojea Masihi arudi. Lakini pamoja na kutoamini kwao kuwa Yesu ndiye, Mungu ameahidi kuwa wao nao wataokolewa na kusamehewa uovu ule wa kumkataa Yesu ( Warumi 11 :25-26).

 

 Yer. 31: 31-34- inaonyesha matengenezo mapya kwa wana wa Israel. Tena watatubu kama taifa na kumkubali Kristo kama Bwana wao! Ezekiel 36:24-29 pia inashuhudia juu ya kuwepo urejesho wa wana wa Israel na kufanywa kwao upya.  Mambo haya yametabiriwa pia katika Zekaria 12:10-11. Maana nyumba ya Israel itamwona Yesu nao watamwombolezea kama taifa zima. Hivyo liko taraja kwa taifa la Israel kihusiana na kumwamini Yesu . Kipindi hicho neema ya wokovu itawageukia zaidi wana wa Israel. Watu wengineo (wa mataifa) wataokoka LAKINI kwa dhiki nyingi!  (Rom.11:25-32) Zamu hii ni zamu ya watu wa Mataifa. Neema ya wokovu imefunuliwa (Tito 2:11-13) Atakaye ipokea atasalimika. Atakaye ikataa ataangamia maana hukumu na gadhabu ya Mungu itamkalia (Yoh.3:36).

Baada ya utangulizi huu, sehemu inayofuata ataangazia juu ya Utawala wa Kristo katika Millenia utakavyokuwa.

 Je utawala wa Kristo wa milenia utakuwa je?

·        Utakuwepo wakati wa AMANI kuu na baraka pote ulimwenguni katika kipindi cha utawala wa Yesu wa Milenia.

·        Dunia itageuzwa na kubadilishwa maana viumbe vya asili vitafunguliwa katika kifungo kilichotokana na dhambi. Ukisoma Warumi 8:19-22, inasema viumbe vinayoshauku (matarajio makuu) ya kufunuliwa  kwa Yesu Kristo. Kwa sasa vinaumia kwa sababu ya dhambi. Maana navyo vitawekwa huru katika utumwa na uharibifu.

·        Isaya 35:1-2 inaonesha jinsi ambavyo katika kipindi hicho Bwana atafanya mambo mengi kuwa mapya. Ezekieli 34:26-27 nayo inathibitisha pia. Maradhi yataondolewa na miaka ya wanadamu itaongezeka. Isaya 35:5-6; na Isaya 65:20-25 inaonesha hilo! Hata mtu wa miaka 100 moja ataonekana kuwa motto. Maandiko yanasema kama zilivyo siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wa Mungu katika kipindi cha milenia ya Kristo!
 

(….itaendelea sehemu ya pili….)

Ni muhimu kutambua mambo haya kwani Kanisa ni wakala wa Ufalme wa Mungu. Wokovu wetu uliandaliwa na Bwana mwenyewe.Ufalme wa Mungu ni wa milele na si wa kitambo kama zilivyo famlme za kidunia! Kanisa , kama wakala wa Ufalme wa mungu, lipo kwa kipindi tu hata ajapo Mfalme mwenyewe, yaani Kristo naye atatawala pamoja na watakatifu. Swali kubwa ni je? Umejiweka tayari? Kama wewe umesoma sehemu hii na ukajiona kuwa umepungukiwa mbele za Mungu, bado iko nafasi kwani mlamgo wa neema uko wazi . Unaweza kutengeneza maisha yako na Mungu kwa kutubu na kumwamini Yesu! Unaweza kuokolewa tu kwa toba na Imani katika Kristo Yesu. Ukimpata Yesu umeupata ufalme maana mwenye ufalme ni Mfame mwenyewe! Leo fanya maamuzi. KUOKOKA NI UAMUZI WAKO!